Skip to content
Back to magazine

(Swahili) Wanakisomo Kibaha Waongoza Mapambano Dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi

29 January 2026
| JAFARI SAIDI MATANGA
| Kibaha District Council
Climate Change ALE

Tanzania

Tanzania

Katika ulimwengu wa sasa, elimu ya watu wazima sio tu kujua kusoma na kuandika; ni nyenzo muhimu ya kujenga uwezo wa jamii kukabiliana na changamoto za kimazingira. Hili lilithibitika mnamo tarehe 27 Januari 2026, ambapo Kituo cha Kujifunzia cha Jamii (CLC) kilichopo Ruvu JKT, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kilifanya zoezi la kihistoria la upandaji miti.

Zoezi hili la upandaji wa miti 100 katika eneo la Shule ya Msingi Ruvu JKT lilifanyika kama sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hata hivyo, tukio hili lilienda mbali zaidi ya sherehe; lilikuwa ni darasa la vitendo kuhusu utunzaji wa mazingira na ujenzi wa ustahimilivu wa jamii.

Mkoa wa Pwani, kama maeneo mengine mengi nchini, unakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazojidhihirisha kupitia ongezeko la joto na uharibifu wa uoto wa asili.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Elimu ya Watu Wazima, Bi. Metrida Kahindi, alisisitiza kuwa elimu inayotolewa kituoni hapo inalenga kuandaa jamii yenye uwezo wa kujilinda na majanga.

"Lengo letu ni kuwafundisha wanakisomo elimu ya utunzaji mazingira kwa vitendo," alisema Bi. Kahindi. "Tunawajengea uwezo wa kuilinda miti hii ili kuifanya Tanzania kuwa ya kijani. Hii ni hatua muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri maisha ya kila siku ya wananchi wetu.”

Zoezi hili linaunganisha dhana ya elimu bila kikomo ambapo wanakisomo wanapojifunza umuhimu wa kupanda miti, wanajifunza namna ya kurejesha uoto wa asili unaosaidia kuhifadhi unyevu wa udongo, kupunguza hewa ya ukaa, na kivuli. Miti iliyopandwa ni kama miti ya matunda na kivuki mfano mizambarau mivule misaplus na mifenesi. Hii inajenga jamii yenye ustahimilivu ambayo inaweza kujitegemea na kuzalisha kwa tija hata wakati wa upungufu wa hewa.

Tukio hili liliungwa mkono kikamilifu na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Ruvu), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, na Mfuko wa Misitu wa Taifa (TaFF). Ushirikiano huu unaonyesha kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la pamoja.

Kupitia Kituo cha Ruvu JKT, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha inaonyesha njia kuwa elimu ya watu wazima ni nguzo imara katika kulinda mazingira kwa ajili ya ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

To add or view comments, please sign up HERE. Already a member? Log in HERE