Skip to content
Back to magazine

(KISWAHILI) ELIMU YA AMALI YAUNGWA MKONO NA WADAU WA ELIMU YA WATU WAZIMA KUPITIA DVV INTERNATIONAL

2 April 2026
| JAFARI SAIDI MATANGA
| Kibaha District Council
ALE

Tanzania

3 I1 A3118

Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la maendeleo ya elimu ya watu wazima, DVV International, imefanya kikao kazi muhimu cha kimkakati kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ili kujadili na kuimarisha utoaji wa Elimu ya Amali (Vitendo) na Elimu ya Watu Wazima (ANFE) kwa wanakisomo.

Kikao hicho kimefanyika leo, Machi 31, 2026, katika Kituo cha Kujifunzia cha Jamii (CLC) kilichopo Shule ya Msingi Ruvu JKT, Kata ya Mtambani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha. Kikao kiliwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa ugani wa kata (Kilimo, Mifugo, na Uvuvi), maafisa maendeleo ya jamii, viongozi wa dini, na wawakilishi wa Asasi za Kiraia (NGOs).

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Mradi kutoka shirika la DVV International, Bw. Michael Mwalupale, amesema wakati umefika wa kuwekeza kwa nguvu katika elimu ya amali inayoendana na miongozo ya ICBAE (Integrated Community-Based Adult Education).

"Lengo letu ni kuhakikisha wanakisomo wanapata ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kujikwamua na tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini, kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, hadi Taifa kwa ujumla," alisema Bw. Mwalupale. Vilevile, alitumia fursa hiyo kutambulisha Jukwaa la Kidijitali la MOJA (MOJA Platform), akiwahimiza wadau kujiandikisha ili kushirikiana, kutangaza kazi zao, na kufanya utetezi wa elimu ya watu wazima kimataifa.

Katika kufanikisha mpango huo, Afisa Elimu ya Watu Wazima wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (DAEO), Bi. Mektilda Kahindi, amesema serikali imejipanga vyema. Amesema ofisi yake inashirikiana kwa karibu na wataalamu wa idara mbalimbali walioko kwenye halmashauri na kata ili kutoa elimu ya vitendo yenye tija kwa wanakisomo, na kuhakikisha mipango hii inaingizwa kwenye bajeti za maendeleo za mitaa.

Kwa sasa, Kituo cha Kujifunzia cha Ruvu JKT (CLC) kinatoa mafunzo mbalimbali ya kiufundi na kijasiriamali ikiwemo: Ufundi Cherehani, Ujasiriamali, Ufugaji wa Samaki, Ufundi Umeme, Kompyuta, na Useremala, yote haya yakienda sambamba na elimu ya msingi ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watu wazima.

Kikao hicho kilimalizika kwa kukubaliana kuunda kamati ya uratibu ngazi ya kata, kuendelea kuhamasisha matumizi ya jukwaa la MOJA, na kuweka mkakati wa pamoja kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kisomo Duniani (International Literacy Day) ili kuendeleza hamasa kwa jamii.

To add or view comments, please sign up HERE. Already a member? Log in HERE